TAWFIQ BLOG |
Katibu
mtendaji wa Necta, Dk Charles Msonde amesema
kuwa “usahihishaji umekamilika na baraza lipo katika uchambuzi wa
kuyapanga na tutakapokamilisha tutayatangaza”.
Alipoulizwa
ni lini hasa matokeo hayo yatatangazwa, Dk Msonde alisema: “Tumemaliza
kusahihisha na mchakato wa kuyapanga ukikamilika tutawaeleza hivyo msiwe
na shaka.”
Katika kipindi cha miaka miwili mfululizo,
mwaka 2012 na 2013, Necta ilitangaza matokeo ya kidato cha nne mwishoni
mwa Februari na mwanzoni mwa Machi.
Matokeo ya Mtihani
wa Kidato cha Nne uliofanyika mwaka 2013 yalitangazwa Februari 22, mwaka
jana na 2012 yalizua gumzo kutokana na asilimia 60 ya watahiniwa
kufeli.
Kwa kawaida, muhula wa masomo kwa kidato cha
tano huanza Julai, huku Machi na Aprili mchakato wa kuwapangia shule
hufanyika wakati Mei na Juni hutumiwa kwa maandalizi kwa wanafunzi hao.
Katika
matokeo ya 2013 kama ilivyokuwa katika matokeo ya mwaka 2012, shule
binafsi zilikuwa na matokeo mazuri kulinganisha na za Serikali
zilizokuwa zikitamba miaka ya nyuma.
Kwa mujibu wa
Necta, matokeo ya mwaka 2013, shule kongwe za Serikali na zile za vipaji
maalumu, zilishindwa kuingia kwenye orodha ya shule 30 bora.
Shule
kongwe kihistoria zimekuwa zikitoka kapa katika matokeo ya Mtihani wa
Taifa. Tofauti na matarajio ya wengi, shule hizo nyingi hazikuwamo hata
katika orodha ya shule 100 bora.
Baadhi ya shule hizo
ni Fidel Castro ambayo ilishika nafasi ya 83, Malangali (172), Ifunda
Ufundi (205), Jangwani (226), Bwiru (242), Songea Wavulana (257), Pugu
(325) na Azania (333).
Ikiwa ni mwaka mmoja umekamilika
tangu Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) ulipoanzishwa, taasisi ya
Hakielimu ilitoa matokeo ya utafiti wake yanayoonyesha hakuna
kilichofanyika.
Kaimu Mkurugenzi wa HakiElimu, Godfrey
Boniventura alisema Serikali isitumie kigezo cha kuongezeka ufaulu kama
ishara tosha ya kuimarika kwa elimu, kwani licha ya ufaulu huu kuonyesha
kupanda ghafla, kuna changamoto nyingi katika sekta hiyo ambazo bado
hazijatatuliwa na juhudi kubwa zinahitajika.
“Mfano
migogoro ya mara kwa mara kati ya walimu na mwajiri, utoro wa walimu,
ukosefu wa maabara, vifaa vya kufundishia na tofauti kubwa iliyopo
katika gharama za utoaji elimu nchini kati ya shule za serikali na shule
za binafsi,” alisema Boniventura.
No comments:
Post a Comment